Afisa Habari wa Yanga Ali Kamwe amesema klabu inajivunia kiungo wake mshambuliaji Stephane Aziz Ki aliyetua kwa Wananchi akitokea klabu ya Asec Mimosas
Kamwe amesema Aziz Ki amekuwa mchezaji muhimu katika kikosi cha Yanga msimu huu na umahiri wake umewasaidia kupata matokeo ya ushindi kwenye baadhi ya mechi
Kumekuwa na maoni tofauti kutoka kwa baadhi ya wachambuzi wa soka nchini kuhusu kiwango cha Aziz Ki lakini kwa mujibu wa takwimu, Aziz Ki msimu wake wa kwanza na Yanga umekuwa bora zaidi pengine kuliko hata msimu wake wa mwisho aliokuwa na Asec Mimosas
"Kupanda na kushuka kunamtokea mchezaji yoyote duniani, kama inaweza kumtokea hata Cristiano Ronaldo au Lionel Messi, basi inaweza kumtokea mwingine yoyote. Tunavyojua Aziz Ki ni mchezaji ambaye anaweza kukupa matokeo chanya, au matokeo yasiyotarajiwa muda wowote ule kwenye mechi yoyote"
"Sitaki kuangalia sijui hajazoea mazingira au msimu wake wa kwanza, lakini alichokifanya tuna kila sababu ya kumpigia makofi kwa sababu amefikisha mabao manane na 'assist' nne, maana yake ameshachangia mabao 12 kwenye Ligi Kuu, achilia mbali mechi za kimataifa. Kwa hiyo licha ya kupanda kwake na kushuka, pamoja na kwamba mnasema hana msimu mzuri, lakini kwenye kikosi chetu hakuna kiungo mwenye namba nzuri kama zake," alisema Kamwe
Katika msimu wake wa kwanza na Yanga, Aziz Ki amefunga mabao 12 na kutoa assist 7 katika mashindano yote
Amepachika mabao 8 ligi kuu, magoli 2 katika michuano ya CAF na magoli mawili kwenye kombe la Shirikisho la Azam (ASFc)
Aziz Ki ametoa pasi nne za mabao ligi kuu, pasi mbili za mabao kwenye michuano ya CAF na pasi moja ya bao kwenye kombe la FA na Ngao ya Jamii
Takwimu hizo ni bora zaidi ya msimu wake wa mwisho akiwa na Asec Mimosas ambapo alifunga mabao 10 na kutoa pasi saba za mabao katika mashindano yote