Katika mchezo wa mkondo wa pili robo fainali ya kombe la Shirikisho barani Afrika kati ya Yanga dhidi ya Rivers United, mkufunzi wa Yanga Nasreddine Nabi alianza na wachezaji saba wazawa
Safu yote ya ulinzi iliundwa na Watanzania kuanzia Dickson Job, Kibwana Shomari, Ibrahim Bacca na Bakari Nondo Mwamnyeto huku Mudathir Yahya na Salum Abubakar 'Sureboy' wakianza kwenye eneo la kiungo na Clement Mzize akianza katika safu ya ushambuliaji
Katika mchezo wa ligi kuu dhidi ya Singida BS ambao Yanga iliibuka na ushindi wa mabao 2-0, Nabi akaanza na safu ileile ya ulinzi yenye wazawa tupu
Unaweza kusema kuanzia kipindi cha pili cha mchezo wa mkondo wa kwanza Shirikisho dhidi ya Rivers United hadi mchezo dhidi ya Singida BS, safu ya ulinzi ya wazawa ilisimama huku wakihakikisha Yanga hairuhusu bao katika mechi tatu zilizopita

Hii ni habari njema kwa timu ya Taifa ya Tanzania 'Taifa Stars' kuelekea mchezo wa kuwania kufuzu Afcon mwezi ujao dhidi ya Niger June 12
Nabi ni kama amemrahisishia kazi kocha wa Stars Adel Amrouche kwa kumtengenezea safu bora ya ulinzi ambayo imepata uzoefu wa kutosha katika mechi hizi za CAF
Uzuri ni kuwa wachezaji wote waliitwa timu ya Taifa katika mechi zilizopita dhidi ya Uganda ambapo wote walipata nafasi ya kucheza
Haitashangaza kuona Yanga ikitoa wachezaji wengi kwenye kikosi cha Stars mwezi Juni kwani wachezaji wake wako katika kiwango bora huku wakicheza mechi nyingi zenye ushindani