Afisa Habari wa Yanga Ali Kamwe amewataka mashabiki wa timu hiyo kuacha kuwasha fataki, moshi na kumulika tochi katika mchezo wa nusu fainali kombe la Shirikisho dhidi ya Marumo Gallants ambao utapigwa Jumatano May 10 katika uwanja wa Benjamin Mkapa
Kamwe ametoa kauli hiyo baada ya Yanga kupigwa faini na Shirikisho la Soka barani Afrika (CAF) kwa matukio ya aina hiyo yaliyojitokeza katika mchezo dhidi ya Rivers United
Kamwe amethibitisha Yanga kupokea barua kutoka CAF inayowataka kulipa fainai dola 35,000 kutokana na matukio yaliyojitokeza wakati wa mchezo dhidi ya Rivers United na kabla ya mchezo ambapo Rivers United walilalamika basi lao kuvamiwa na kuibiwa kiasi cha dola 5200 wakati wakikamilisha mazoezi ya mwisho uwanja wa Benjamin Mkapa
"Tumepokea barua yenye maelekezo kutoka CAF, ikitutaka tulipe faini dola 35,000 kutokana na matukio yaliyojitokeza katika mchezo dhidi ya Rivers United. Uongozi wa Yanga utakutana leo kujadili adhabu hiyo kwani tumepewa nafasi ya kukata rufaa kama tunadhani sio sahihi"
"Lakini jambo muhimu nawaambia Wananchi wenzangu tuache kupiga fataki, kuwasha moto, moshi na kumulika tochi wakati wa mechi kwani tutafungiwa"
"Baadhi ya Matukio yanafanywa sana na wenzetu waarabu lakini huoni wakiadhibiwa hivyo Wananchi tunawaomba waache hizi tabia kwasababu tupo hatua nzuri ambayo inawezekana tunajaribiwa kutolewa kwenye 'focus' tunaomba Wananchi waache hizi tabia ili tusiwape sababu," alisema Kamwe