Afisa Habari wa Yanga Ali Kamwe amewataka mashabiki wa timu hiyo kujitokeza kwa wingi kwenye uwanja wa Azam Complex, Chamazi katika mchezo wa ligi kuu dhidi ya Dodoma Jiji ambao utapigwa kesho Jumamosi, May 13 2023 saa 10 jioni
Kamwe amesema hii ni mechi maalum ya ubingwa kwa Yanga hivyo wanapaswa kujitokeza kwa wingi kwa ajili ya shamrashamra za baada ya dakika 90
Hata hivyo Kamwe amesema ili Yanga kutwaa ubingwa lazima ishinde mchezo huo, wingi wa mashabiki utaongeza morali ya wachezaji katika kusaka ushindi
"Hii ni mechi ya ubingwa kwa sababu kama tutashinda itakuwa rasmi tumetetea ubingwa wetu kwa msimu wa pili mfululizo. Nawaomba mashabiki mje kwa wingi kwani kutakuwa na shamrashamra kabla na baada ya mchezo"
"Burudani itaanza saa sita mchana, siku ya kesho huu uwanja wa Azam Complex utakuwa wetu kwa siku nzima, hivyo kata tiketi yako mapema, uwanja unachukua mashabiki wachache"
"Baada ya mchezo kutakuwa na matukio ya aina mbalimbali. Mashabiki watakuwa na nafasi ya kuwaona wachezaji na viongozi wakiwa na familia zao. Kutakuwa na tukio la shukrani kutoka kwa wachezaji kwenda kwa mashabiki katika kutambua mchango wao kwa timu," alisema Kamwe
Kamwe amesema Yanga itaondoka jijini Dar es salaam Alfajiri ya Jumapili kuelekea Afrika Kusini kwa ajili ya mchezo wa mkondo wa pili nusu fainali ya kombe la Shirikisho dhidi ya Marumo Gallants
Amesema pamoja na ushindi wa mabao 2-0 waliopata kwenye mchezo wa kwanza nyumbani, bado wana kazi ya kufanya Afrika Kusini ili kuhakikisha wanatinga fainali
"Bado tunahitaji dua na maombi yenu Wananchi, mechi hii ya pili itakuwa ngumu zaidi. Marumo Gallants ni timu nzuri, katika uwanja wao wa nyumbani timu iliyofungwa mabao machache ni Pyramids tu iliyofungwa bao moja. Hivyo tunajua ni kiasi gani tunakabiliwa na mchezo mgumu huko kwao lakini lengu letu ni kuhakikisha tunashinda na kutinga fainali"
"Mwaka huu tunataka kufanya jambo kubwa kwa kulileta kombe la Shirikisho Tanzania"