Mshambuliaji wa Yanga Fiston Mayele amesema kitu pekee ambacho wachezaji wanafikiria ni kutwaa kombe la Shirikisho barani Afrika na kuingia katika vitabu vya kumbukumbu
Yanga itacheza fainali ya michuano hiyo wakianza na mchezo wa mkondo wa kwanza dhidi ya USM Alger utakaopigwa Jumapili May 28 katika uwanja wa Benjamin Mkapa na timu hizo kurudiana Juni 03 nchini Algeria
Mayele anayeongoza orodha ya vinara wa mabao katika michuano hiyo akiwa amefunga mabao 6, amesema hii ni mechi ya kufa au kupona, hawako tayari kupoteza nafasi adimu ya kushinda taji hilo
"Akili zetu zote zipo katika mchezo muhimu unaowakilisha Taifa na nguvu zetu tumeweka huko ili kuhakikisha tunafanya vizuri"
"Kambini kwetu kwa sasa kila mmoja anatamani kuona tunatwaa ubingwa na hayo ndiyo mazungumzo ambayo yamekuwa yakitawala"
"Wakati mwingine tukipeana mbinu za hapa na pale kuhakikisha tunapata ushindi kwenye mchezo wa fainali, kila mmoja amekuwa akimhimiza mwenzake kuhakikisha anafanya vizuri"
"Fainali yoyote siyo rahisi ndio maana tunafanya maandalizi makubwa ili kuhakikisha tunafanya vizuri na kurudisha heshima kikosini kwetu," alisema Mayele
Yanga inahitaji kushinda mchezo wa mkondo wa kwanza Jumapili ili kuwa na nafasi ya kutwaa taji hilo katika mchezo wa marudiano utakaopigwa wiki ijayo