Kikosi cha Yanga kinaendelea na maandalizi kuelekea mchezo wa mkondo wa pili fainali ya kombe la Shirikisho barani Afrika dhidi ya USM Alger ambao utapigwa Jumamosi, Juni 03 huko Algeria
Yanga inakabiliwa na ratiba ya aina yake kwani itafunga msimu huu wa mashindano kwa kucheza mechi nne katika muda wa siku 9!
Baada ya fainali ya pili dhidi ya USM Alger, Yanga inapaswa kurejea Tanzania mara moja na kuunganisha mkoani Mbeya ambako wanakabiliwa na mchezo wa ligi kuu dhidi ya Mbeya City Juni 06
Siku tatu baadae hapohapo Mbeya, Juni 09 Yanga itashuka tena uwanja wa Sokoine kuikabili Tanzania Prisons katika mchezo ambao Wananchi watakabidhiwa taji la ligi kuu ya NBC
Baada ya mchezo huo Yanga itaelekea mkoani Tanga ambako siku tatu nyingine Juni 12 wanakabiliwa na mchezo wa fainali kombe la Shirikisho la Azam (ASFC) dhidi ya Azam Fc ambao utapigwa uwanja wa Mkwakwani
Tangu Juni 03 mpaka Juni 12 Yanga itacheza mechi nne ndani ya muda wa siku tisa tu
Kwa ratiba hii ni wazi kocha mkuu wa Yanga Nasreddine Nabi anaweza kulazimika kutumia baadhi ya wachezaji wa kikosi cha kwanza na timu ya vijana katika mechi dhidi ya Mbeya City na Tanzania Prisons ili wachezaji wengine wapate mapumziko kuelekea mchezo wa fainali ya FA dhidi ya Azam Fc