Mshambuliaji wa Yanga kinara wa mabao Fiston Mayele amesema wanakwenda Algeria wakiwa na dhamira moja tu, kusaka ushindi katika mchezo wa mkondo wa pili fainali ya kombe la Shirikisho dhidi ya USM Alger
Mayele amesema watacheza mchezo huo wakiwa hawana presha yoyote akiamini presha itakuwa kwa wapinzani wao
"Mechi ya kwanza tulicheza uwanja wa Benjamin Mkapa tulikuwa na presha kubwa. Mashabiki walikuwa wamejaa na wanataka ushindi. Lakini sasa itakuwa zamu yao USM Alger nao kuwa na presha kucheza mbele na mashabiki wao"
"Sisi hatuna wasiwasi wowote kucheza kwenye uwanja uliojaa ugenini, mimi nimeshiriki mechi nyingi za aina hiyo, tutajitolea kwa nguvu zetu zote ili kuhakikisha tunashinda na kurudi Tanzania na kombe," alisema Mayele muda mfupi kabla ya kuanza safari ya Algeria
Msafara wa watu takribani 250 umeondoka leo kuelekea Algeria ukijumuisha wachezaji 29 wa Yanga, baadhi ya viongozi wa Yanga, Wizara ya Michezo ikiongozwa na Waziri Pindi Chama, mashabiki na wadau wa soka waliopata nafasi ya kujumuishwa katika safari hiyo