Haikuwa bahati kwa Yanga kushinda taji la Shirikisho msimu huu lakini ni wazi mchezo wa pili wa fainali dhidi ya USM Alger jana umeonyesha ni kwa kiasi gani Yanga iko tayari kulikamata soka la Afrika
USM Alger walilazimika kutumia kila aina ya mbinu kushinda taji katika mchezo wa fainali ambao kwa hakika wengi waliotizama hawakufurahishwa na matukio waliyoyaona
Walianza kwa kuvamia Hotel waliyofikia Yanga usiku mnene na kuwapa wachezaji usumbufu kwa kupiga fataki na kelele ikiwa ni mbinu ya kuwafanya wasipate utulivu
Kilichotokea uwanjani ilikuwa aibu zaidi, pengine mpira ulichezwa kwa dakika 60 tu, dakika 30 zilipotea kwa matukio ya kupoteza mda
Wachezaji wa USM Alger kujiangusha, fataki na vijana wa kuokota mipira kuchelewesha muda kwa kutorudisha mipira uwanjani inapotoka au kurudisha mpira zaidi ya mmoja. Haya ni matukio yaliyochukua muda mwingi zaidi wa mchezo
Wachezaji wa Yanga wanastahili pongezi kwa kushinda mchezo katika mazingira magumu sana, bahati tu haikuwa upande wao kutwaa taji
Ilikuwa kosa kukubali kupoteza mchezo nyumbani, matokeo yale ndio yaliyoikosesha Yanga kombe. Lakini Yanga ilikuwa bora katika mchezo wa pili na kupata ushindi katika mazingira ambayo sio rahisi kwa mgeni
Kocha Nasreddine Nabi na benchi lake la ufundi pia wanastahili pongezi kwa kufanikiwa kimbinu katika mchezo wa jana. Ukiona timu inatumia mbinu zisizo za kimpira katika mchezo basi fahamu mambo yalikuwa magumu kwao
Wananchi wamevaa medaki rasmi za CAF, itabaki kuwa kumbukumbu kwa vizazi na vizazi
Wachezaji warudi nyumbani wakiwa kifua mbele kwani hakuna deni kwao, wamepambana bahati haikuwa upande wao