Ligi Kuu ya NBC msimu wa 2022/23 inafika tamati leo kwa mabingwa wateule Yanga kushuka uwanja wa Sokoine mkoani Mbeya kumenyana na Tanzania Prisons
Katika msimu wa pili mfululizo Yanga itakabidhiwa taji la Ligi Kuu mkoani Mbeya kwani baada ya dakika 90 za mchezo huo tukio litakalofuata ni wananchi kukabidhiwa 'mali' yao
Ni mchezo unaotarajiwa kuwa na upinzani mkali, Tanzania Prisons haijawahi kuwa timu nyepesi inapokutana na Yanga pamoja na kuwa kila timu imeshapata kile ilichohitaji
Tanzania Prisons wana uhakika wa kucheza ligi kuu msimu ujao wakati Yanga ni mabingwa kwa msimu wa pili mfululizo
Hata hivyo Wananchi wanahitaji ushindi na hasa mshambuliaji Fiston Mayele kupachika mabao ambao yatamuhakikishia ufungaji bora
Msimu huu Mayele anastahili kuwa mfungaji bora na kwa hakika leo wachezaji wenzake watamsaidia kuhakikisha anashinda tuzo hiyo
Mchezo utaanza mapema saa 9:30 ili kupisha muda wa shamrashamra za ubingwa