Mshambuliaji wa Yanga Fiston Mayele pengine msimu huu anaweza kuondoka na tuzo ya mfungaji bora licha ya kufungana mabao na Saido Ntibazonkiza wa Simba
Bao alilofunga katika mchezo dhidi ya Tanzania Prisons leo limemfanya Mayele afikishe mabao 17 sawa na Saido ambaye amefunga mabao mawili katika mchezo dhidi ya Coastal Union
Kamati ya tuzo itakaa kuamua mchezaji ambaye anapaswa kushinda tuzo hiyo lakini kwa kuangalia vigezo vya msimu uliopita, Mayele anaweza kushinda
Kabla ya mechi ya mwisho msimu uliopita, Mayele na George Mpole walikuwa wamefunga mabao 16 kwa kila mmoja ambapo TFF ilibainisha kuwa kama wangemaliza na idadi sawa ya mabao basi kigezo cha kwanza kuangaliwa ni idadi ya mabao ya penati ambapo mchezaji aliyefunga mabao machache ya penati ananufaika
Msimu huu mabao yote 17 aliyofunga Mayele hakuna bao la penati wakati Saido ana mabao matatu ya penati
Kigezo pekee ambacho kinaweza kumnyima Mayele tuzo hiyo ni kama iwapo wataangalia 'assist'
Saido ametoa jumla ya assist 12 akiwa na klabu za Geita Gold na Simba pia akifunga mabao 17 akiwa na timu za Simba na Geita Gold
Mabao ya Mayele yana thamani kubwa zaidi kwa sababu yameisaidia Yanga kushinda ubingwa wa Ligi Kuu na haya ndio mafanikio makubwa zaidi kwa timu