Klabu ya Yanga imesema hatma ya aliyekuwa kocha wake msaidizi Cedric Kaze, itafahamika mara baada ya kupatikana kwa Kocha Mkuu
Kaze amemaliza mkataba wake na Yanga lakini bado hakuna mazungumzo yaliyofanyika baina yake na uongozi wa Yanga hasa baada ya aliyekuwa Kocha Mkuu Nasreddine Nabi kuondoka
Afisa Habari wa Yanga, Ali Kamwe, amesema kwa sasa wapo kwenye mchakato wa kumpata Kocha Mkuu na atakapokabidhiwa majukumu ndiye atakayeamua kuendelea kufanya kazi na benchi lililopo akiwamo Kaze, au kuja na watu wake.
"Sasa hivi mazungumzo yaliyopo ni kumpata kocha mkuu, tukishampaka ndiyo tunampa fursa mwalimu anayekuja kuchagua wasaidizi wake, akitoa ruhusa tutaendelea na mazungumzo, yeye ndiye atakayetuambia watu gani anaotaka kufanya nao kazi kwenye benchi lake la ufundi"
"Akisema anawahitaji sawa, lakini anaweza kusema anakuja na benchi lake la ufundi, ndiyo dunia ya mpira wa sasa ilipofikia na sisi Yanga ni weledi," alisema Kamwe
Kumekuwa na taarifa kuwa Kaze anasubiri kuungana na Nabi katika majukumu ya klabu mpya (Kaizer Chiefs) ambayo anatarajiwa kujiunga nayo
Hata hivyo imeelezwa kuwa Kaizer Chiefs wamegomea mapendekezo ya Nabi kwenda na baadhi ya wataalam wake aliokuwa nao Yanga jambo ambalo limefifisha matumaini ya Kaze kuibukia Kaizer Chiefs