Ujio wa mshambuliaji Hafiz Konkoni umeongeza vita katika safu ya ushambuliaji ya Yanga
Katika misimu miwili iliyopita, Fiston Mayele alijipambanua na kujihakikishia nafasi ya kuanza katika kikosi cha kwanza
Baada ya Mayele kuondoka ni wazi Kocha Mkuu wa Yanga Miguel Gamondi anahitaji kufanya maamuzi ya kuchagua mshambuliaji kiongozi kati ya Kennedy Musonda, Clement Mzize na Konkoni
Vita kubwa itakuwa kati ya Konkoni na Musonda ambaye anaamini baada ya Mayele kuondoka ni zamu yake kuuteka ufalme wa Jangwani
Musonda alimaliza vyema msimu uliopita akifunga bao pekee la Yanga kwenye mchezo wa fainali kombe la FA dhidi ya Azam Fc lakini pia akarejea na makali yake akifunga bao la Yanga kwenye mchezo kilele cha wiki ya Mwananchi dhidi ya Kaizer Chiefs
Juzi katika mchezo wa kirafiki dhidi ya Magereza DSM ambao Yanga iliibuka na ushindi wa mabao 10-0, Musonda alifunga hat-trik sawa na Mzize
Kama ilivyo kwa wachezaji wengi wapya, Konkoni huenda akahitaji muda kuzoea mazingira lakini hapana shaka katika uwezo wake

Msimu uliopita kwenye ligi kuu ya Ghana, akiitumikia Benchem United, Konkoni alipachika mabao 15 katika mechi 26 huku akitoa pasi tatu za mabao
Tofauti na Musonda, Konkoni ni mshambuliaji wa kati (striker) na hupendelea zaidi kucheza namba 9
Musonda ana faida zaidi kwa kuwa anaweza kutumika kama winga. Pengine katika baadhi ya mechi Musonda na Konkoni wote wanaweza kuanza kama ilivyokuwa kwa Mayele na Musonda
Hata hivyo katika moja ya mahojiano yake, Musonda alisema msimu ujao atapenda atumike zaidi kama namba 9 kwani ndio nafasi ambayo anapendelea zaidi kuicheza