Mshambuliaji Clement Mzize juzi ni kama aliwatumia salamu washambuliaji wenzake katika kikosi cha Yanga Kennedy Musonda na Hafiz Konkoni
Ulikuwa mchezo wa nusu fainali ya Ngao ya Jamii dhidi ya Azam Fc uliopigwa uwanja Mkwakwani Yanga ikiibuka na ushindi wa mabao 2-0 na kutinga fainali
Katika mchezo huo Mzize ambaye alicheza kwa takribani dakika 30, alifunga bao la pili, kuingia kwake kulibadili mwenendo wa mchezo
Baada ya Fiston Mayele kuondoka ni kama Kocha Mkuu wa Yanga Miguel Gamondi hajapata mshambuliaji wake namba moja ingawa katika mechi dhidi ya Azam Fc alianza na Musonda
Konkoni hakutumika katika mchezo huo kwa kuwa bado anaimarisha utimamu wa mwili pengine Wananchi huenda wakamshuhudia katika mchezo wa fainali dhidi ya Simba siku ya Jumapili
Ni wazi kwa kiwango bora alichoonyesha Mzize, anaweza kumshawishi Gamondi kuanza nae kwenye mchezo dhidi ya Simba
Pamoja na kufunga bao, Mzize alifanya majaribio manne, mawili yalikwenda nje huku moja likigonga mwamba
Dakika zake 30 zilikuwa bora zaidi kulinganisha na Musonda ambaye walinzi wa Azam Fc walimuwekea ulinzi mkali
Ni mwanzo mzuri kwa Mzize, mechi ya Jumapili inaweza kumuhakikishia nafasi kwenye kikosi cha kwanza kama ataaminiwa na kufanya zaidi ya kile alichofanya katika mchezo dhidi ya Azam Fc