Majira ya saa 1 usiku leo, mchezo wa fainali Ngao ya Jamii kati ya Yanga dhidi ya Simba utapigwa uwanja wa Mkwakwani
Ni msimu wa tatu mfululizo timu hizo zinachuana kuwania Ngao ya Jamii, Yanga ikiibuka na ushindi katika misimu miwili iliyopita
Kwa mara ya kwanza mwaka huu, michuano ya Ngao ya Jamii imehusisha timu nne, ikianzia hatua ya nusu fainali
Yanga ilitinga fainali kibabe kwa ushindi wa mabao 2-0 dhidi ya Azam Fc wakati wapinzani wao Simba walilazimika kusubiri mikwaju ya penati kupata ushindi dhidi ya Singida FG katika mchezo ambao uligubikwa na malalamiko mengi kwa mwamuzi Amina Kyando
Ni fainali nyingine ambayo inapigwa nje ya jiji la Dar es salaam baada ya ile ya kombe la Shirikisho la Azam (ASFC) iliyopigwa Kigoma miaka miwili iliyopita
Yanga ilionyesha kiwango bora katika mchezo dhidi ya Azam Fc, matumaini ni makubwa kwa Wananchi kuwa leo timu yao ina nafasi kubwa ya kuibuka na ushindi
Hata hivyo mara nyingi mechi za derby huwa hazitabiriki, pamoja na kuwa Simba walionekana kuwa chini katika mchezo dhidi ya Singida FG, leo wanaweza kuwa tofauti
Kocha Mkuu wa Yanga Miguel Gamondi anajivunia ubora wa kikosi chake, timu yake ikiwa na muunganiko mzuri
Mechi itakuwa ngumu lakini Wananchi wana kila sababu ya kwenda uwanjani kifua mbele kwani wana timu bora