Kocha Mkuu wa Yanga Miguel Gamondi amesema kikosi chake kiko tayari kwa mchezo wa ligi kuu dhidi ya KMC ambao utapigwa kesho Jumatano katika uwanja wa Azam Complex
Licha ya kutopata muda wa kutosha wa maandalizi baada ya mchezo wa ligi ya mabingwa dhidi ya Asas Fc, Gamondi amesema wanafahamu aina ya mchezo wanakwenda kukabiliana nao
"Ratiba sio rafiki sana kwa sababu tumecheza Jumapili, lakini kama timu kubwa tunapaswa kujiandaa na kupata matokeo mazuri katika kila mechi"
"Nimewaona KMC kwenye mchezo wao waliocheza Jumamosi (dhidi ya Namungo), ni timu nzuri natarajia utakuwa mchezo mzuri"
"Naamini kwa umoja wetu na sapoti ya mashabiki tutakuwa na mchezo mzuri utakaoambatana na soka safi la ushindani," alisema Gamondi
Kuhusu hali za wachezaji baada ya mchezo dhidi ya Asas Fc, Gamondi amesema baadhi walipata changamoto ndogo lakini anaamini baada ya mazoezi ya mwisho leo watakuwa tayari kwa mchezo huo
Akizungumza kwa niaba ya wachezaji wenzake, winga Denis Nkane amesema baada ya kupoteza Ngao ya Jamii, jukumu lao wachezaji ni kuhakikisha wanaanza vyema msimu ili kutetea mataji yote yaliyobaki