Licha ya kugawa vipigo kwa timu pinzani, Kocha Mkuu wa Yanga Miguel Gamondi amesema kikosi chake bado hakijafikia ubora ambao anataka
Gamondi amesisitiza kuwa bado anahitaji muda kuendelea kukiimarisha kikosi chake akiwataka mashabiki wa Yanga waendelee kuwa wavumilivu
"Unaweza kusema tumefika kutokana na mtazamo wa haraka na matokeo tunayopata lakini kimbinu na kiufundi kulingana na falsafa yangu bado kabisa hatujafika pale ninapotaka. Tunatakiwa kuwa bora na kuweza kudumu katika ubora huo kwa msimu wote"
"Kila kitu kipo hapa cha kutufanya tuwe bora. Tuna uongozi bora , mashabiki wenye upendo na timu yao na kikosi chenye mseto mzuri kuweza kukifanya kuwa bora uwanjani. Hatuhitaji kuridhika sasa kwani bado mapema, mtazamo wa kuridhika kwangu haupo labda msimu ukiisha"
"Muda wote tunapaswa kuwa na kiu ya kushinda na mchezo bora pia," alisema Gamondi
Gamondi ameiongoza Yanga katika mechi 5 za mashindano akishinda mechi nne na kupoteza mchezo mmoja kwa mikwaju ya penati (Ngao ya Jamii) baada ya matokeo ya suluhu ya bila kufungana dhidi ya Simba
Katika mechi hizo tano, Yanga imeruhusu bao moja tu huku wakifunga mabao 14