Septemba 16 Yanga itakuwa uwanja wa Pele Rwanda kumenyana na El Merrikh katika mchezo wa mkondo wa kwanza kuwania tiketi ya kutinga hatua ya makundi ligi ya mabingwa barani Afrika
Mchezo huo kupigwa Rwanda ni habari nzuri Wananchi kwani hakuna shaka Yanga itapata uungwaji mkono mkubwa kutoka kwa mashabiki
Kutokana na historia yake, Yanga itakapokuwa Rwanda ni kama itakuwa nyumbani tu
Rais wa Rwanda Paul Kagame ni mdau mkubwa wa michezo na inaaminika kuwa ni shabiki mkubwa wa Yanga
Mwaka 2012 Rais Kagame aliialika Yanga nchini Rwanda baada ya kuwa imetwaa taji la Kagame. Hii mialiko ya Marais kwa Wananchi ilianza siku nyingi....!
Lakini pia ukizungumzia kizazi cha wachezaji bora wa Rwanda hutakosa kumtaja Haruna Niyonzima ambaye kucheza kwake Yanga kwa muda mrefu kuliwafanya mabingwa hao wa Tanzania Bara kupata umaarufu mkubwa huko Rwanda
Wananchi wa Rwanda watakuwa na shauku kubwa ya kuiona Yanga baada ya miaka mingi kupita tangu ilipocheza nchini humo
Pia uongozi wa Yanga unatarajiwa kuandaa usafiri kwa mashabiki kutoka Tanzania ambao watapenda kusafiri na timu Rwanda kwa ajili ya kuongeza hamasa
Msimu huu Yanga imepania kutinga hatua ya makundi ya michuano ya ligi ya mabingwa na mkakati ni kuhakikisha mchezo unamalizikia hukohuko Rwanda