Kocha Mkuu wa Yanga Miguel Gamondi ameeleza kuvutiwa na uwezo unaoonyeshwa na wachezaji wote katika kikosi chake
Yanga imesajili wachezaji 28 msimu huu ambapo wachezaji wote wametumika katika mechi za kirafiki huku 26 wakitumika katika mechi za mashindano
Gamondi amebainisha kuwa kuna ushindani mkubwa katika kiwanja cha mazoezi kila mchezaji akipambana ili kupewa nafasi kwenye kikosi cha kwanza na hivyo kumfanya awe na jeshi kubwa la kulitumia katika mechi mbalimbali
Licha ya kutokuwepo kwa mastaa 11 wa timu hiyo walioitwa kwenye timu za taifa, zinazojiandaa na mechi za kuwania kufuzu fainali za Afrika (Afcon) 2023 zitakazofanyika Ivory Coast, wengi wao wakiwa wa kikosi cha kwanza, lakini Gamondi ametahadharisha kwamba hadi sasa hakuna mwenye uhakika wa namba kikosini
Gamondi amesema mpaka sasa hana kikosi cha kwanza, ataendelea kutumia wachezaji wake kwa kuliangana na aina ya mpinzani wanayecheza nae
"Pamoja na timu kupata matokeo mazuri kwenye michezo tuliyocheza hadi sasa bado sijapata wachezaji wa kikosi cha kwanza kutokana na nafasi za wachezaji nilionao kila mmoja kuonyesha uwezo na kuhitaji kucheza kwenye kikosi hicho, hivyo Yanga kila mmoja ana nafasi ya kucheza kulingana na timu tunayokutana nao," alisema Gamondi
Katika kikosi cha Gamondi haishangazi mchezaji kufanya vizuri mechi moja na kujikuta yuko jukwaani katika mechi inayouata huku mchezaji aliyechukua nafasi yake akiuwasha moto vilevile
Gamondi amefanya mabadiliko katika kila nafasi kuanzia golikipa mpaka namba 11 lakini timu yake ikaendelea kucheza katika kiwango kilekile