Kikosi cha Yanga Princess kinaendelea na mazoezi kwa ajili ya maandalizi ya msimu ujao wa Ligi Kuu ya Wanawake na mashindano ya Get International, huku akisisitiza kuwa wanataka ubingwa
Wiki iliyopita Yanga Princess iliachana na wachezaji 13, imefanya usajili bora zaidi unaowajumuisha nyota wa kigeni akiwemo Madina Traore kiungo kutoka Burkina Faso, Faiza Sedu straika raia wa Ghana na Adejoke Ejalonibu kiungo mshambuliaji kutoka Raja Casablanca ya Morocco.
Kocha Msaidizi wa Yanga Princess Fred Mbuna amesema viongozi wa Yanga waliona haja ya kuondoa wachezaji 13 ili kuimarisha kikosi kwa ajili ya msimu ujao na anaamini wapya waliosajiliwa watasaidia kutwaa ubingwa
Msimu uliopita Yanga Princess ilimaliza katika nafasi ya nne kwenye msimamo wa ligi.
Yanga Princess ilicheza mechi mbili za kirafiki wiki iliyopita ile ya kwanza ikishinda mabao 7-0 dhidi ya Sports Academy na 2-0 dhidi ya Ilala Queens ikiwa ni kipimo cha maandalizi ya michuano ya Get International yatakayofanyika mjini Dodoma kuanzia Septemba 9 hadi 23.
Mashindano hayo yanajumuisha timu 12 zikiwamo Get Program, Fountain Gate Princess, Yanga Princess, Simba Queens, Bunda Queens, New Generation, JKT Queens, Alliance Girls, CFC Aman FC, Polisi Queens, Kampala Queens na Ceasia Queens.