Yanga inatumia uwanja wa Azam Complex kwa mechi zake za nyumbani wakati huu ambao uwanja wa Benjamin Mkapa umefungwa kwa ajili ya maboresho
Unaweza kusema ulikuwa uamuzi sahihi kwa uongozi wa Yanga kuchagua uwanja wa Azam Complex kwani katika msimu huu hakuna timu imetoka salama mbele ya Yanga kwenye mechi zote zilizochezwa katika uwanja huo
Yanga ni kama imejimilikisha uwanja huo, hata wamiliki halali Azam Fc wameshindwa kuvuna kile ambacho Yanga wamekivuna kwani waliondoshwa katika kombe la Shirikisho hapo hapo
Yanga imeshinda mechi zote tano ilizocheza katika uwanja huo katika mashindano yote msimu huu
Ushindi katika mechi mbili za ligi ya mabingwa dhidi ya Asas Fc na ushindi katika mechi tatu za ligi kuu dhidi ya KMC, JKT Tanzania na Namungo Fc
Jumla ya mabao 18 yamefungwa huku Wananchi wakiruhusu bao moja tu kutikisa nyavu zao
Kesho Jumamosi Septemba 30 Wananchi wanashuka tena uwanja wa Azam Complex kuikabili Al Merrikh katika mchezo wa mkondo wa pili kuwania kufuzu hatua ya makundi ligi ya mabingwa barani Afrika
Yanga itaingia uwanjani ikiwa na lengo moja tu, kusaka ushindi ili kuongezea katika mtaji wa mabao mawili waliyofunga katika mchezo wa mkondo wa kwanza
Ni wazi utakuwa mchezo mgumu lakini mpaka sasa hakuna timu imetoka salama mbele ya Yanga hapo Azam Complex