Yanga itaanza kampeni ya hatua ya makundi michuano ya ligi ya mabingwa barani Afrika msimu huu kwa kuumana na CR Belouizdad katika mchezo wa kwanza kundi D ambao utapigwa Novemba 25 huko Algeria
Hii itakuwa mara ya pili kwa Yanga kwenda Algeria baada ya msimu uliopita kwenda kuchuana na USM Alger kwenye mchezo wa fainali kombe la Shirikisho (CAF CC) Yanga ikiibuka na ushindi wa bao 1-0
Habari njema kwa Yanga ni kuwa katika benchi la ufundi kuanzia kocha Miguel Gamondi wanafahamu kipi kitapaswa kufanyika kwenye mchezo huo ili kuhakikisha Yanga inaanza vyema kampeni yake ya kusaka robo fainali
Gamondi amewahi kuinoa klabu ya CR Belouizdad na mwenyewe amebainisha kuwa ni furaha kwake kurejea tena Algeria lakini wakati huu akiwa na Wananchi
"CR Belouizdad ni timu yangu ya zamani. Nilipata wakati mzuri sana nikiwa nao. Wana mashabiki wengi na wanaipenda timu yao kama ilivyo kwa Yanga"
"Ni timu yenye historia inayofanana na Yanga kwani nao walipigania Uhuru wa Algeria. Nafikiri utakuwa mchezo mzuri dhidi yao, Tutakuwa na muda mzuri wa kujiandaa na bila shaka tutakwenda Algeria kupambana ili kuhakikisha tunapata matokeo mazuri," alisema Gamondi
Jana timu hiyo ilitangaza kumtimua aliyekuwa Kocha wake Mkuu Sven Vandenbroeck baada ya kuchezea kichapo kwenye ligi kuu ya Algeria. Vandenbroeckh amewahi kufundisha Simba ya Tanzania