Mchezo wa ligi kuu dhidi ya Simba siku ya Jumapili utaamuliwa na mbinu za kocha Miguel Gamondi pamoja na ari, upambanaji wa wachezaji katika kuzisaka alama tatu
Yanga inahitaji kushinda mchezo huu ili kuendelea kubaki kileleni mwa msimamo wa ligi katika kampeni ya kusaka ubingwa wa tatu mfululizo
Wananchi wataingia katika mchezo huo wakiwa na kumbukumbu ya kupoteza mechi mbili zilizopita dhidi ya Simba
Msimu uliopita Yanga ilipoteza mchezo wa kwanza wa ligi kuu dhidi ya Simba baada ya miaka mitatu
Ulikuwa ni mchezo ambao ulimalizika kwenye kipindi cha kwanza, magoli ya mapema yalivuruga mipango ya aliyekuwa kocha mkuu Nasreddine Nabi na kukubali kipigo cha mabao 2-0
Wakati huu Yanga inakwenda katika mchezo huo ikiwa katika ubora mkubwa lakini bado wachezaji watahitaji kuwa na nidhamu
Mechi hii itakuwa tofauti na ile ya Ngao ya Jamii, huenda mchezo ukawa wa wazi zaidi kuliko wakati ule ambao Simba walibaki basi
Mchezo kuwa wazi maana yake kutakuwa na nafasi nyingi zinazoweza kutengenezwa, katika mechi ambazo Simba wamecheza msimu huu wapinzani wametengeneza nafasi nyingi dhidi yao na wamefunga mabao pia
Kwa kasi waliyonayo viungo washambuliaji wa Yanga Stephane Aziz Ki, Maxi Nzengeli na Pacome Zouzoua, ni wazi kutakuwa na nafasi nyingi za kufunga
Kibu Denis ndiye mchezaji ambaye safu ya ulinzi ya Yanga itahitaji kuwa nae makini kwani kwa sasa ndiye anayeonekana kusukuma mashambulizi ya Simba
Pengine Gamondi anaweza kumuhitaji 'mbishi' Kibwana Shomari katika mchezo huo kwa kazi maalum ya kumdhibiti Kibu
Kasi na soka la mabavu inaweza kuwa changamoto kwa Joyce Lomalisa ambaye hata kwenye mchezo wa Ngao ya Jamii Gamondi alilazimika kumtoa na nafasi yake kumuingiza Nickson Kibabage baada ya purukushani za Kibu aliyeingia kipindi cha pili