Jana majira ya usiku, Yanga iliwasili mkoani Tanga tayari kwa mchezo wa ligi kuu dhidi ya Coastal Union
Mchezo huo utapigwa kesho Jumatano, Novemba 08 katika uwanja wa Mkwakwani
Meneja wa Yanga Walter Harrison amesema wamefuata alama tatu mkoani Tanga
"Tunashukuru timu imesafiri salama na kufika Tanga, tunasubiri siku ya Jumatano kuikabili Coastal Union"
"Wachezaji wote wako kwenye hali nzuri, ari ya morali iko juu dhamira ikiwa kuendelea kuwapa furaha Wananchi baada ya ushindi mnono dhidi ya Simba"
"Coastal Union hawajafanya vizuri katika mechi zao msimu huu lakini mara nyingi wanapokutana na Yanga katika uwanja wa Mkwakwani mechi huwa haitabiriki"
"Sisi tumejiandaa kukabiliana nao na kama nilivyosema awali, malengo yetu ni kushinda mchezo huo," alisema Walter
Baada ya ushindi dhidi ya Simba, Wananchi wamejichimbia kileleni mwa msimamo wa ligi wakifikisha alama 21
Ushindi katika mchezo dhidi ya Coastal Union utawafanya waendelee kujiongezea alama kileleni mwa msimamo