Zilikuwa wiki tatu ngumu kwa Yanga zilizoambatana na mfululizo wa mechi ngumu hata hivyo Yanga imetoka salama ikifanikiwa kuvuna alama tatu katika kila mchezo
Mwezi Oktoba haukuanza vyema kwa Yanga ikipoteza mchezo wa kwanza wa ligi kuu msimu huu kwa kufungwa mabao 2-1 ugenini dhidi ya Ihefu Fc
Licha ya kipigo hicho Yanga haikuyumba, ikaenda kupata ushindi wa mabao 3-0 dhidi ya Geita Gold mkoani Mwanza. Wananchi wakarejea jijini Dar es salaam kukabiliana na ratiba yenye mtego
Walianza na Azam Fc Oktoba 23 Yanga ikaibuka na ushindi wa mabao 3-2. Wakapumzika siku tatu, siku ya nne wakarudi tena uwanja wa Benjamin Mkapa kumenyana na Singida FG Yanga ikifanikiwa kuibuka na ushindi wa mabao 2-0
Wiki moja baadae, Wananchi wakarudi tena dimba la Mkapa kuchuana na watani zao wa jadi Simba na wakashusha kipigo cha mbwa mwizi cha mabao 5-1 kipigo ambacho kimepeleka kilio Msimbazi na kupelekea kocha kutimuliwa na bado tuhuma za kusalitiana zikiendelea kuvuma
Baada ya mchezo huo uliopigwa Jumapili, Wananchi hawakuwa na muda wa kupumzika kabisa kwani Jumatatu wakaondoka Dar kuelekea Tanga kwa ajili ya mchezo dhidi ya Coastal Union uliopigwa jana na Yanga kuibuka na ushindi wa bao 1-0
Ilikuwa ratiba iliyoibua malalamiko miongoni mwa Wananchi wakiitaka Bodi ya Ligi kuwa na huruma kwani wachezaji sio robot
Watani zao Simba ambao walichuana nao Jumapili, walipewa muda wa kutosha kupumzika wao wako Dar na watacheza dhidi ya Namungo Fc leo
Ikumbukwe pia Simba ilipewa wiki nzima kujiandaa na mchezo dhidi ya Yanga, mechi yao dhidi ya Mashujaa iliwekwa kiporo na haijulikani wataicheza lini
Aidha mwishoni mwa mwezi huu Simba ilipaswa kucheza na Azam Fc baada ya mchezo wao wa kwanza wa hatua ya makundi ligi ya mabingwa lakini tayari mechi hiyo imepigwa kalenda hadi mwezi Januari 2024!
Ni wazi msimu huu utakuwa mgumu sana kwa Yanga lakini pongezi kwa wachezaji na benchi la ufundi kwani wanajitoa kwa kila namna ili kuwapa furaha Wananchi