Licha ya kulazimishwa sare ya bao 1-1 dhidi ya Al Ahly, Kocha Mkuu wa Yanga Miguel Gamondi amesema bado nafasi ya kufuzu robo fainali ipo
Gamondi amesema wanarejea mazoezini kujiandaa na mchezo unaofuata dhidi ya Medeama ambao watahitaji kushinda ugenini
Kocha huyo raia wa Argentina alisema malengo yao ilikuwa kushinda mchezo dhidi ya Al Ahly nyumbani lakini haikuwa hivyo
"Hayakuwa matokeo mazuri kwetu kwani malengo yetu yalikuwa kushinda lakini yatupasa tusonge mbele, bado nafasi ya kufuzu hatua ya robo fainali ipo"
"Nawapongeza wachezaji wangu, licha ya kuruhusu bao kwenye dakika za mwisho hawakukata tamaa na kuweza kusawazisha"
"Ulikuwa mchezo ambao kama tungekuwa makini kwenye kipindi cha kwanza tungetumia nafasi nyingi tulizotengeneza"
"Kipindi cha pili Al Ahly walikuwa bora, mpira ni mchezo wa makosa, tulifanya kosa wakalitumia kutuadhibu"
"Tunarejea katika uwanja wa mazoezi kufanya kazi, tuna siku chache za kusahihisha mapungufu tuliyoyaona katika mchezo uliopita ili kuhakikisha tunapata ushindi mchezo unaofuata," alisema Gamondi
Hesabu za Yanga ni kushinda mechi mbili zinazofuata dhidi ya Medeama ili kuweka hai matumaini ya kutinga robo fainali
Ni wazi mechi hizo zitakuwa ngumu lakini ili kupata mafanikio katika michuano hii ni lazima kushinda mechi ngumu