Kocha Mkuu ya Yanga Miguel Gamondi amesema winga Skudu Makudubela pamoja na wachezaji wengine katika kikosi chake wana nafasi sawa ya kucheza lakini ni lazima waonyeshe wanastahili nafasi hiyo
Kumekuwa na maoni tofauti kutoka kwa mashabiki wa Yanga kwenye mitandao ya kijamii baadhi wakihoji kutotumika kwa baadhi ya wachezaji akiwemo Skudu
Gamondi amesema Skudu ni mchezaji mzuri na anafurahi kufanya nae kazi kikosini akiamini hata yeye ana furaha kuitumikia klabu ya Yanga
"Skudu ni mchezaji mzuri katika kikosi chetu, yeye na wachezaji wengine wote wana nafasi sawa katika timu. Alipata majeraha katika mchezo wetu wa kwanza msimu huu na kupelekea akawa nje ya uwanja kwa takribani wiki tatu hadi nne"
"Sasa amepona kabisa majeraha na anaendelea kufanya mazoezi kama ilivyo kwa wachezaji wengine, changamoto imekuwa kurejea kwenye kikosi cha kwanza kwa sababu kuna wachezaji wanafanya vizuri zaidi"
"Skudu anafahamu hili, bado ni mchezaji muhimu kwetu, na sio yeye tu, tuna wachezaji wengine saba ambao nao wanapambana kwenye uwanja wa mazoezi, kila mmoja wakati wake wa kucheza utafika," alisema Gamondi
Skudu huenda akapewa nafasi ya kuanza katika mchezo wa ligi kuu dhidi ya Mtibwa Sugar utakaopigwa Jumamosi uwanja wa Azam Complex
Gamondi anatarajiwa kufanya mabadiliko ya kikosi chake baada ya mechi tatu ngumu za hatua ya makundi ligi ya mabingwa