Oktoba 04 2023 uwanja wa Highland Estates, Mbarali mkoani Mbeya, Yanga ilikubali kichapo cha mabao 2-1 dhidi ya Ihefu Fc katika mchezo wa Ligi Kuu ya NBC
Ni kipigo ambacho hakikutarajiwa mapema katika msimu huu ikizingatiwa Yanga ilianza 'kibabe' msimu kwa kugawa vipigo vya tano tano
Zuberi Katwila ndiye aliyekuwa Mkufunzi wa Ihefu Fc wakati huo ambapo baada ya ushindi alitamba kuwa anaifahamu vyema Yanga na haikuwa ngumu kuifunga
Mara kadhaa wakati mchezo ukiendelea Katwila alionekana akitunishiana misuli na benchi la ufundi la Yanga ambao walikerwa na mbinu za kupoteza muda zilizokuwa zikitumiwa na wachezaji wa Ihefu kwa maelekezo ya Katwila ambaye baadae aliadhibiwa na Kamati ya saa 72 ya Bodi ya Ligi
Katwila sasa anainoa Mtibwa Sugar na Jumamosi ataiongoza timu hiyo katika mchezo wa ligi kuu dhidi ya Yanga utakaopigwa uwanja wa Azam Complex
Kwa kocha Miguel Gamondi, mchezo huu una umuhimu wa kipekee dhidi ya Katwila, kudhihirisha kuwa alipoteza mchezo kule Mbarali kwa bahati mbaya na sio kuzidiwa kimbnu
Aidha Gamondi anafahamu mazingira atakayokutana nayo katika mchezo huo pengine hayatakuwa tofauti na yale aliyokutana nayo Mbarali
Pengine kutakuwa na matukio mengi ya kupoteza muda ili kuwaondoa wachezaji wa Yanga mchezoni kama ilivyokuwa mechi dhidi ya Ihefu
Hata hivyo Katwila na kikosi chake wanakwenda kukabiliana na Yanga tofauti katika dimba la Azam Complex
Katika uwanja huo Yanga imeshinda mechi zote tatu, ikifunga jumla ya maba0 11 pasipo kuruhusu bao
Katika uwanja huo KMC alipigwa 5-0, JKT Tanzania akapigwa 5-0 kisha Namungo Fc wakapigwa 1-0
Mchezo wao wa mwisho Mtibwa Sugar katika uwanja wa Azam Complex dhidi ya Azam Fc, walipigwa 5-0, sasa wanarejea tena katika uwanja huo dhidi ya Yanga