Kocha Mkuu wa Yanga Miguel Gamondi amesema kikosi chake kiko tayari kwa mchezo wa ligi kuu dhidi ya Mtibwa Sugar ambao utapigwa kesho Jumamosi katika uwanja wa Azam Complex
Akizungumza katika Mkutano na wanahabari, Gamondi amesema amekuwa na wiki nzuri ya maandalizi na hivyo anaamini watakuwa na mchezo mzuri hapo kesho
"Nafurahi tumepata wiki moja ya mazoezi hivyo naamini tutakuwa na mchezo mzuri hapo kesho. Tutawakosa baadhi ya wachezaji kutokana na sababu mbalimbali ikiwemo kutumikia adhabu na majeruhi. Lakini pia tunapaswa kuwa na tahadhari kwani tunakabiliwa na mchezo wa ligi ya mabingwa," alisema Gamondi
Katika hatua nyingine Gamondi amesema jambo muhimu kwa sasa ni kuona timu yake inacheza vizuri na kushinda mechi
Gamondi amesisitiza kila mchezaji kwake ana umuhimu, nani anacheza na nani yuko nje hutegemea na mpango wa mchezo na utayari wa wachezaji
Ameeleza sababu kwa nini baadhi ya wachezaji hawapati nafasi na pia uamuzi wake wa kutotumia mawinga
"Nahitaji kutengeneza timu ambayo inacheza pamoja na kutengeneza nafasi, kufunga mabao pia"
"Wakati mwingine nalazimika kucheza bila winga kwa sababu tukitumia winga hatutengenezi nafasi nyingi. Lakini tunao wachezaji viungo (MAP) ambao wametengeneza nafasi nyingi na kufunga mabao"
"Kama kocha napaswa kuamua, msimu uliopita tulikuwa na Mayele (Fiston) aliyekuwa katika kiwango cha juu (alifunga mabao 30+). Fikiria timu hii ingekuwa na Mayele ingekuwa wapi? Sasa hayupo Mayele hivyo tunatengeneza timu ambayo inacheza pamoja na kutengeneza nafasi nyingi," alisema