Jambo pekee ambalo kocha anapaswa kudaiwa ni matokeo mazuri ya timu yake na sio vinginevyo
Upo msemo kuwa makocha wanaajiriwa ili wafukuzwe, ndivyo ilivyo, pale timu inapokosa matokeo chanya basi maisha ya kocha katika timu hiyo yanafika ukingoni
Hivyo sio sahihi kwa mashabiki kumpangia kocha wachezaji wa kuwatumia wakati kama atafanya hivyo na timu yake ikakosa matokeo mazuri ni yeye atakayefukuzwa
Jana kocha Miguel Gamondi aliwakumbusha mashabiki wa Yanga kilichotokea kwenye mchezo dhidi ya Ihefu Fc baada ya yeye kufanya 'rotation'
Mashabiki walimgeuka na kuona hakuwa sahihi kubadili timu yake ya ushindi, iweje leo waone anakosea kwa kutobadilisha timu yake ya ushindi?
Nafikiri Wananchi hawapaswi kuingia katika mtego ambao yawezekana watani zao wanatamani wanase
Huyu Gamondi sio mtu mzuri kwao! Ni siku 40 zimepita tangu awashushie kipigo cha aibu pale uwanja wa Benjamin Mkapa
Mijadala mingi inayoanzishwa huko mitandaoni na wanaojitambulisha kuwa ni mashabiki wa Yanga ambao hawafurahishwi na Gamondi kutofanya 'rotation' ni uongo
Ni wajanja wanaojaribu kuchochea moto kumchonganisha Gamondi na wachezaji wake na kuutega uongozi wa Yanga umtimue
Mpaka sasa Yanga haijafanya vibaya chini ya Gamondi. Katika mechi 18 za mashindano yote, Yanga imepoteza michezo miwili na kutoka sare miwili
Sare mbili na kipigo kimoja ni katika mechi za Ligi ya Mabingwa ambazo ushindani wake ni wa juu kuliko mechi za ndani
Yanga imeruhusu mabao 10 ambapo kati ya mabao hayo, matano imefungwa kwenye ligi ya mabingwa
Gamondi anafahamu ni wakati gani amtumie mchezaji yupi ili timu yake ipate matokeo mazuri hivyo ni vyema akaachwa afanye kazi yake