Kikosi cha Yanga kinarejea mazoezini leo Avic Town kwa ajili ya maandalizi ya mchezo wa ligi ya mabingwa dhidi ya Medeama Fc
Meneja wa Kitengo cha Habari na Mawasiliano Ali Kamwe amesema kutokana na umuhimu wa mchezo huo, hakutakuwa na mapumziko kwa wachezaji
"Leo ni Jumapili, kwa kawaida leo wachezaji walipaswa kupewa mapumziko baada ya mchezo dhidi ya Mtibwa Sugar jana lakini kutokana na umuhimu wa mchezo dhidi ya Medeama Fc hakutakuwa na mapumziko"
"Wachezaji wanarudi mazoezini saa 11 jioni kuanza maandalizi ya mchezo huo. Tunashukuru wachezaji wote wapo salama, watakuwa Avic Town jioni kushiriki mazoezi," alisema Kamwe
Kamwe amesema wapinzani wao Medeama Fc watawasili nchini kwa makundi uongozi wa timu hiyo umetoa taarifa ya ujio wao
NI GSM DAY
Kamwe ametangaza kuwa mchezo dhidi ya Medeama Fc utakuwa maalum kwa ajili ya Mdhamini/Mfadhili wa Yanga Ghalib Said Mohammed 'GSM' ambaye amenunua tiketi zote za Mzunguuko (tiketi 45,000) kwa ajili ya mashabiki kujitokeza kwa wingi kuipa hamasa timu yao
"Tumekuwa na kawaida ya kuwa na siku za wachezaji, sasa tumekuja kiutofauti, mdhamini na mfadhili wetu Ghalib Said Mohamed amenunua tiketi zote za mzunguko. Hivyo mechi ya Medeama FC tunakwenda kwa jina la GSM Day kuthamini mchango wake kwenye mchezo huu"
"Je kwenye siku ya GSM Day tunatokaje? Ili kuheshimisha siku ya tajiri? Namna pekee ya kumuonesha tunathamini mchango wa GSM, siku ya jumatano hakikisha unakuja na jezi ambayo imetengenezaa na GSM. Ukija na jezi chupli hutaruhusiwa kuingia uwanjani"
"Mtu akiwauliza kwanini tajiri wetu anatununulia tiketi, muulize kwani huyu ni boss wenu? Muulize una wivu? Muulize unaumia? Muulize unakwazika? Kwani wao pia si wana tajiri? Mwambieni awanunulie," alisema Kamwe
Kamwe amesisitiza kuwa malengo ya Yanga ni kushinda mchezo huo ili kujiwekea mazingira mazuri ya kufuzu robo fainali
"Lengo letu la kwanza ilikuwa kutinga hatua ya makundi ya ligi ya mabingwa. Wengi walitubeza kuwa inakuwaje timu kubwa inaweka malengo haya? Sisi tulikwenda na uhalisia. Tulipofika kwenye makundi tukaweka lengo la pili ni kufuzu robo fainali baada ya kufanya tathmini ya kundi. Hatuweki malengo kwa mihemko. Na tutafanikisha lengo letu la pili inshallah"