Ikiwa tayari imetinga robo fainali ya michuano ya kombe la Mapinduzi, kesho Yanga itakamilisha ratiba ya michuano hiyo kwa mchezo wa mwisho wa hatua ya makundi dhidi ya KVZ
Kocha Msaidizi wa Yanga Mussa Ndaw amesema watautumia mchezo huo kuwapa nafasi wachezaji ambao hawakupata dakika nyingi katika michuano hiyo
"Kwanza tumefurahishwa na kiwango kilichoonyeshwa na timu yetu hapo jana. Wachezaji walipambana mpaka dakika ya mwisho tukafunga bao la ushindi"
"Tayari tumetinga robo fainali hivyo tutautumia mchezo dhidi ya KVZ kuwapa nafasi wachezaji ambao hawakucheza dakika nyingi katika mechi zilizopita, na wengine wakirejea kutoka kwenye majeruhi"
"Ni mechi ambayo mashabiki watawashuhudia Augustine Okrah, Shekhan Khamis, Joyce Lomalisa na hata baadhi ya wachezaji kutoka timu yetu ya vijana ambao hawakuwaona katika mechi zilizopita," alisema
Yanga ilifanikiwa kutinga robo fainali jana baada ya ushindi wa mabao 2-1 dhidi ya Jamus Fc
Wananchi ndio vinara wa kundi C wakiwa na alama sita na mabao saba ya kufunga huku wakiruhusu bao moja