Wakati siku tano zikiwa zimesalia kabla ya dirisha dogo la usajili kufungwa, Yanga inatarajiwa kupitisha panga kali kwa kuachana na wachezaji ambao hawaendani na mahitaji ya timu
Rais wa Yanga Injinia Hersi Said juzi katika mahojiano maalum na Clouds Fm, aliweka wazi kuwa hawatamuangalia mchezaji usoni kama hana msaada kwa timu
Hersi alisema hakutakuwa na presha kwa viongozi au benchi la ufundi kwa mchezaji ambaye ameshindwa kutimiza majukumu yake uwanjani kwa sababu hafai kuwa mchezaji wa timu hiyo
"Katika usajili tunaofanya matarajio yetu ni kuona mchezaji anatupa matokeo uwanjani, kama hawezi uwanjani hakuna sehemu nyingine atatuonyesha uwezo, hivyo hakuna nafasi kwake," alisema Hersi
Yanga iko kwenye majadiliano na mshambuliaji Hafiz Konkoni ambaye ameshindwa 'kuingia kwenye mfumo' huku kukiwa na taarifa kuwa nyota wengine wawili wa kigeni wanaweza kuondoka
Wachezaji wengine wa kigeni ambao hawajawa na mwendelezo mzuri katika kikosi cha kocha Miguel Gamondi ni pamoja na Gift Fred, Jesus Moloko na Skudu Makudubela
Chrispine Ngushi, Jonas Mkude na Denis Nkane nao wako kwenye hatihati baada ya kukosa nafasi katika kikosi cha Gamondi