Jana Yanga ilifunga dirisha la usajili kwa utambulisho wa mshambuliaji Joseph Guede raia wa Ivory Coast aliyetua Jangwani kuchukua nafasi ya Hafiz Konkoni aliyetolewa kwa mkopo
Safari yake ya soka ilianza akiwa na klabu ya USC Bassam mnamo 2017-2018, na kisha akaendelea kuonyesha ujuzi wake na kung'ara zaidi katika msimu wa 2018-2019 akiwa na AFAD Djekanou.
Mnamo Agosti 1, 2018, Joseph Guede alisajiliwa FAR de Rabat ambapo katika msimu wake wa kwanza aliwashangaza wengi kwa uwezo wake wa kupachika mabao na kutoa pasi za mabao
Guede alithibitisha zaidi uwezo wake katika msimu wa 2019/2020 akiwa mchezaji muhimu wa FAR Rabat. Alimaliza msimu huo akiwa mfungaji bora wa klabu yake na magoli 10 kwenye ligi, huku klabu yake ikimaliza msimu katika nafasi ya sita ya ligi.
Mnamo Desemba 15, 2020, aliendeleza rekodi yake ya mafanikio kwa kufunga bao lake la kwanza msimu huo katika ushindi wa 2-0 dhidi ya Rapide Club d'Oued-Zem
Guede akiwa na FAR Rabat na Emirates Fc ambayo aliitumikia kwa mkopo wa msimu mmoja, alifunga jumla ya mabao 26 na assist 12 katika mechi 91
Baada ya mkataba wake na FAR Rabat kumalizika, Guede alielekea Uturuki ambapo aliitumikia Tuzlaspor inayoshiriki ligi daraja la kwanza akidumu na timu hiyo kwa muda mfupi kabla ya kuvunja mkataba wake kwa kilichoelezwa kukiukwa kwa makubaliano
Guede pia amewahi kujumuishwa katika kikosi cha timu ya Taifa ya Ivory Coast na alipata nafasi ya kucheza mechi moja
Akiwa na umri wa miaka 29, Joseph Guede tayari ni mchezaji mwenye uzoefu mkubwa na pasipo na shaka Wananchi watarajie makubwa kutoka kwake