Kikosi cha Yanga kimeingia wiki ya pili ya mazoezi Avic Town Wananchi wakijiweka sawa wakati huu ambao ligi imesimama kwa ajili ya michuano ya Afcon 2023
Baadhi ya mastaa wa Yanga wameeleza mwenendo wa maandalizi hayo yanayosimamiwa Master Miguel Gamondi na benchi lake la ufundi
"Tupo kwenye morali nzuri na ya ushindani ukizingatia kuna maingizo mapya hivyo tunapambana kuhakikisha tunajiweka kwenye hali ya ushindani ili kuhakikisha kila mmoja anakuwa fiti tayari kwa mapambano," mshambuliaji Clement Mzize alinukuliwa na Mwanaspoti
Nae kiungo Mganda Khalid Aucho amesema wanaendelea vizuri na mazoezi na kila mchezaji anajua nini anafanya kwa ajili ya ligi itakaporudi huku akisisitiza kuwa walipoishia hautakuwa mwanzo na kwamba zaidi watarudi kivingine katika mashindano.
"Yanga ina malengo yake na ndio tunayoyapambania kwa kujiweka tayari kwa kushindana na washindani wetu ili kuweza kufikia malengo bila ya kuhofia ubora utatokana na sisi kujiandaa na kuwa imara kwa changamoto zote zitakazokuwa mbele yetu," alisema Aucho ambaye atakosa mchezo wa ligi kuu utakaofuata kutokana na kutumikia adhabu ya kadi nyekundu akiwa tayari amekosa mechi mbili
Beki Joyce Lomalisa alisema yupo fiti na tayari kwa kuipambania timu yake baada ya kutoka kwenye changamoto ya majeraha amerudi kwenye ushindani akicheza mechi mbili za mashindano ya Mapinduzi
Yanga inawakosa wachezaji saba ambao wako Ivory Coast kushiriki michuano ya Afcon 2023. Stephane Aziz Ki na Djigui Diarra tayari wamejihakikishia kuendelea kubaki Ivory Coast kwa muda zaidi baada ya mataifa ya Burkina Faso na Mali kujihakikishia kucheza hatua ya mtoano
Nyota wanne wanaocheza timu ya Taifa ya Tanzania na Kennedy Musonda wa Zambia hatma yao itafahamika baada ya mechi zitakazopigwa leo