Baada ya kuiongoza Yanga kutinga robo fainali ya michuano ya ligi ya mabingwa barani Afrika, Kocha Mkuu wa Yanga Miguel Gamondi amesema wanaelekeza nguvu zao katika mechi za ligi kuu ili kuhakikisha Yanga inatetea ubingwa kwa msimu wa tatu
Gamondi ameingia katika vitabu vya kumbukumbu vya Yanga baada ya kumaliza miaka 25 ya Wananchi kusubiri kucheza hatua ya makundi ya ligi ya mabingwa akiwahakikishia kucheza robo fainali
Gamondi amesema yeye na benchi la ufundi wanajisikia fahari kwa kuiwezesha Yanga kufikia mafanikio hayo lakini bado kazi haijamalizika sasa wakiweka nguvu kwenye mechi za ligi kuu wakati wakisubiri droo ya robo fainali
"Haikuwa rahisi kufikia malengo lakini imewezekana kutokana na umoja na ushirikiano kuanzia benchi la ufundi, wachezaji, viongozi na mashabiki"
"Nafurahi kuwa sehemu ya historia ya klabu hii, miaka 25 ni mingi, lakini wakati huu tumefanikiwa na tunayo nafasi ya kufanya vizuri zaidi"
"Tunarudi kwenye ligi tunakabiliwa na ratiba ngumu ya mechi mfululizo lakini dhamira yetu ni kuona tunafanya vizuri ili tuwape furaha mashabiki wetu ambao wamekuwa nasi kila wakati," aalisema Gamondi
Mchezo unaofuata kwa Yanga ni dhidi ya Namungo Fc utapigwa Ijumaa, March 08 uwanja wa Majaliwa, Lindi
Yanga iko kileleni mwa msimamo wa ligi ikiwa na alama 43 sawa na Azam Fc inayoshika nafasi ya pili kwa tofauti ya mabao
Hata hivyo Azam Fc wamecheza mechi 19 wakati Yanga ina mechi 16 tu