Mapokeo ya droo ya robo fainali ya ligi ya mabingwa ambapo Yanga imepangwa kucheza dhidi ya Mamelodi Sundowns yamebainisha taswira za aina mbili
Sehemu kubwa ya mashabiki wa Yanga wameipokea droo hiyo kwa mikono miwili wakiweka imani kuwa hakuna jambo lisilowezekana katika mpira wa miguu
Lakini lipo kundi jingine la mashabiki ambao wameingia hofu na kukosa imani juu ya nafasi ya Yanga kufuzu hatua ya nusu fainali
Pengine hawa wameingia 'kwenye mfumo' wa watani zao ambao tangu Yanga ilivyopangwa na Mamelodi Sundwons wamefurahia wakiamini hakuna nafasi kwa Yanga kufuzu nusu fainali
Ukifuatilia mashabiki wa Mamelodi nao wamefurahia droo hiyo wakiamini ni njia rahisi kwao kwenda nusu fainali. Lakini lipo kundi la mashabiki wachache ambao wanaamini mechi haitakuwa rahisi kutokana na ubora wa Yanga
Hawa ni wale walioifuatilia Yanga tangu msimu uliopita ilipocheza fainali ya kombe la Shirikisho na msimu huu ilivyofanikiwa kutinga robo fainali ya CAF CL
Hii inaweza kuwa nafasi nnzuri kwa Yanga kuwaduwaza mabingwa hao wa Afrika Kusini ambao wanasaka taji la pili la CAF CL
Mara ya mwisho Mamelodi kushinda taji la Ligi ya Mabingwa ni mwaka 2016 wakati huo wakinolewa na Pitso Mosemane
Yawezekana aina ya soka wanalocheza ndilo linalowatisha wengi lakini wana taji moja tu la ligi ya mabingwa ambalo walichukua miaka nane iliyopita
Katika misimu miwili iliyopita Mamelodi waliishia hatua za robo fainali na nusu fainali. Msimu wa 2021/22 walitolewa na Petro Atletico kwenye robo fainali na msimu uliopita wakatolewa nusu fainali na Wydad iliyoifunga Simba kwa matuta hatua ya robo fainali
Msimu huu Mamelodi walishinda taji la AFL ambalo lilifanyika kwa mara ya kwanza wakicheza fainali dhidi ya Wydad ambao katika ligi ya mabingwa hawakuweza hata kutinga robo fainali
Ukiangalia takwimu za Yanga katika michuano ya CAF tangu msimu uliopita, utaona hawa Mamelodi ni mpinzani mzuri sana kwani nao wanatabia za Yanga
Mamelodi wamekuwa wakifanya vizuri ugenini kitu ambacho Yanga wamefanya. Kimbinu wanaonekana ni timu inayopata matokeo katika ardhi ya ugenini wakitumia presha ya mwenyeji kusaka ushindi nyumbani
Wenyewe mashabiki wa Mamelodi wanasema ukiona timu yao imekuachia umiliki mpira ujue ni mtego huo, wanakuvia upoteze mpira katika maeneo hatarishi wakumalize kupitia 'counter-attack'
Pengine hili ndio jambo ambalo Kocha Miguel Gamondi anapaswa kulichukulia tahadhari pale timu hizo zitakapokutana kwenye mchezo wa kwanza uwanja wa Benjamin Mkapa
Kama Yanga itafanikiwa kupata ushindi nyumbani ni wazi watakuwa na nafasi ya kutinga nusu fainali kwani mechi ya pili presha itakuwa upande wa Mamelodi ambao mara nyingi katika mechi za mtoano wanakosa clean-sheet nyumbani