Kocha Mkuu wa Yanga Miguel Gamondi amesema vijana wake wako tayari kwa mchezo wa ligi kuu dhidi ya Azam Fc ambao utapigwa kesho Jumapili katika uwanja wa Benjamin Mkapa
Akizungumza katika Mkutano na Wanahabari kuelekea mchezo huo, Gamondi amesema hizi ni aina ya mechi ambazo ushindi unaweza kuwaweka katika nafasi nzuri ya kutwaa ubingwa
Hata hivyo Gamondi amesema wachezaji wake wanapitia wakati mgumu kutokana na mfululizo wa mechi lakini anaamini kesho watakuwa tayari kuipambania Yanga na kuhakikisha wanaibuka na ushindi
"Kesho tutakuwa na mchezo mzuri sana kwa sababu timu zote mbili zinacheza soka safi, Azam FC wameonesha ukomavu wa hali ya juu msimu huu hivyo tuna kila sababu ya kujituma sana"
"Licha ya ugumu wa ratiba bado tunayo njaa ya kupata alama tatu, hizi ni aina ya mechi ambazo unahitaji alama tatu kujiweka katika nafasi nzuri ya kushinda ubingwa, najua wachezaji wangu wanapitia nyakati ngumu kutokana na uchovu lakini nawahakikisha wanachi tutapigana mpaka tone la mwisho," alisema Gamondi
Akizungumza kwa niaba ya wachezaji wenzake, mshambuliaji Clement Mzize amesema, wachezaji wote wako timamu kiafya tayari kuwapa burudani Wananchi
"Kiafya wachezaji wote tupo na afya njema, tunawasihi wananchi wajitokeze kwa wingi kwani tunawahakikishia tutapambana, tunafahamu Azam FC ni timu ngumu na wametupa upinzani mkubwa mara kadhaa lakini Yanga SC ni timu kubwa hatupaswi kuwa na hofu"