Wapinzani wa Yanga katika mchezo wa robo fainali ligi ya mabingwa barani Afrika, Mamelodi Sundowns wanatarajiwa kuwasili nchini kesho Alhamisi
Meneja wa Habari na Mawasiliano klabu ya Yanga Ali Kamwe amethibitisha ujio wa Sundowns hapo kesho huku akiwataka mashabiki wao ambao wako hapa nchini waende JNIA kuipokea timu yao hapo kesho
Akizungumza na Wananchi jana katika shamra-shamra za hamasa kuelekea mchezo huo, Kamwe alisema Yanga iko tayari kwa mechi kubwa inayosubiriwa Afrika nzima siku ya Jumamosi
"Afrika inajua mechi kubwa ni moja tu ambayo ni Young Africans SC na Mamelodi. Kila mwafrika anaizungumzia mechi hii. Hii ndio mechi ambayo imetikisa zaidi AFRIKA kwa sasa. Huu ni muda wetu, na hii ni mechi ya Muda. Hii ndio timu kubwa nchi hii. Tutavuka kwenda nusu fainali kwa soka safi"
"Hao mnaowaita Wabrazil watambe wanakotambaga lakini kwenye ardhi hii hakuna wa kututambia. Tunatamba wenyewe anayebisha aseme yeye ametamba mbele yetu? Suala la kupandisha mnara hatutanii tunapandisha kwa yeyote"
"Sisi hatuna vita na Mamelodi, hatuwachukii, kama wapo wengi waje kwa wingi uwanjani. Young Africans SC lugha yetu ni amani, hatupigi wala kuzuia mtu kuja kwa Mkapa. Kama mnataka kwenda kuwapokea ndugu zenu nendeni wanafika Alhamisi. Ugomvi wetu na Mamelodi utakuwa kwenye Dakika 90 Uwanjani. Wote mnakaribishwa kwa Mkapa," alisema Kamwe