Bodi ya Ligi Kuu imewahakikishia usalama mashabiki watakaojitokeza uwanja wa Benjamin Mkapa Jumamosi katika mchezo wa dabi ya Kariakoo kati ya Yanga dhidi ya Simba
Akizungumza na waandishi wa Habari leo, Afisa habari wa Bodi ya Ligi (TPLB), Karim Boimanda amesema tayari wamezungumza na watu wa ulinzi na usalama kwa ajili ya kuweka usalama kwenye mchezo huo unaotarajiwa kushuhudiwa na mashabiki wengi
"Hadi sasa tumezungumza na watu wa ulinzi juu ya kudhibiti matukio mbalimbali kwenye mchezo huo mkubwa Afrika Mashariki na kati" alisema Boimanda
Tiketi za mchezo huo zimeendelea kuuzwa kwa kasi kubwa mashabiki wa Yanga wakionekana kuhamasika zaidi kununua tiketi kuliko watani zao Simba
Meneja wa Habari na Mawasiliano wa Yanga Ali Kamwe ametamba kuwa siku ya Jumamosi itakuwa kama kilele cha wiki ya Mwananchi kwani wamedhamiria kujaza dimba la Mkapa peke yao kipindi hiki ambacho mashabiki wa Simba 'wamesusa'
Mchezo huo wa mkondo wa pili ligi kuu ya NBC utapigwa kuanzia saa 11 jioni