Meneja wa Habari na Mawasiliano klabu ya Yanga Ali Kamwe bado anatafuta eneo zuri ambalo litafaa bango la 7-2 kukaa!
Ni baada ya ushindi wa mabao 2-1 ambao Yanga waliupata dhidi ya watani zao Simba katika mchezo wa ligi kuu uliopigwa uwanja wa Benjamin Mkapa hivyo kuwafanya Wananchi kupata ushindi wa jumla wa mabao 7-2 dhidi ya watani zao hao katika mechi mbili za ligi
Ulikuwa mchezo wa kuweka rekodi kwa Yanga kwani katika kipindi cha miaka 10, ni mara ya pili Yanga inapata ushindi katika mechi zote mbili za ligi kuu dhidi ya SimbaΒ
Mara ya mwisho ilifanya hivyo msimu wa 2015/16 ikishinda kwa mabao 2-0 katika mechi zote mbili wakati huo ikiwa chini ya kocha Hans Van Pluijm
Lakini pia Aziz Ki aliweka rekodi ya kufunga katika mechi zote mbili, kwani pia alifunga bao katika ushindi wa mabao 5-1 ambao Yanga iliupata katika mchezo wa duru ya kwanza
Aziz Ki sasa ameingia katika rekodi ya wachezaji ambao wamefunga mabao matatu au zaidi katika mechi za watani wa jadi
Ki pia ameendeleza rekodi ya kibabe dhidi ya Simba akiwa sasa amewafunga mabao matano tangu akiwa Asec Mimosas
Katika katika mchezo huo pia kulikuwa na mfungaji mpya, Joseph Guede aliyefunga bao la pili kwa uhodari wa hali ya juu
Baada ya kusajiliwa dirisha dogo, Guede alianza majukumu yake na Yanga taratibu lakini kwa sasa amedhihirisha ni mshambuliaji hatari
Lilikuwa bao lake la tatu kwenye ligi msimu huu yote akiyafunga katika mechi mbili zilizopita
Mpaka sasa Guede tayari amepachika mabao sita katika mashindano yote