Meneja wa Yanga Walter Harrison amewataka mashabiki kujitokeza kwa wingi uwanja wa Meja Jenerali Isamuhyo kuipa hamasa timu yao katika mchezo wa ligi kuu dhidi ya JKT Tanzania utakaopigwa kesho
Walter amesema Yanga inakaribia kukamilisha malengo yake ya kutwaa ubingwa msimu huu, hivyo kipindi hiki inawahitaji sana mashabiki wake ambao wamekuwa bega kwa bega na timu tangu msimu ulipoanza
"Baada ya mapumziko ya siku moja, leo tumerejea mazoezini kukamilisha maandalizi ya mchezo dhidi ya JKT Tanzania ambao utapigwa kesho (Jumanne) katika uwanja wa Meja Jenerali Isamuhyo"
"Wachezaji wote wako tayari kwa mchezo huo isipokuwa Joyce Lomalisa ambaye alipata changamoto kidogo katika mchezo uliopita dhidi ya Simba"
"Tunawaomba mashabiki wetu mjitokeze kwa wingi uwanja wa Meja Jeneral Isamuhyo, Mbweni jijini Dar es salaam kama mlivyofanya katika mechi zilizopita msimu huu"
"Tumekaribia kukamilisha malengo yetu ya kutwaa ubingwa, hivyo tunaomba mje kwa wingi muwaongezee hamasa wachezaji wetu katika kuhakikisha tunafanikisha jambo letu," alisema Walter
Kimahesabu Yanga inahitaji kushinda mechi tano katika mechi nane zilizobaki ili kutawazwa kuwa mabingwa wa ligi kuu kwa msimu wa tatu mfululizo