Ushindi wa bao 1-0 dhidi ya Mashujaa Fc, umewasogeza Wananchi karibu zaidi na ubingwa wa ligi kuu msimu huu
Yanga imefikisha alama 65 huku ikiwa na mechi tano za kuhitimisha msimu huu. Wananchi wanahitaji alama nane tu kukamilisha hesabu za ubingwa pasipo kujali matokeo ya wapinzani wake Azam Fc na Simba
Lakini pia ushindi huo umeziongezea presha Azam Fc na Simba ambazo zitachuana katika mchezo ambao unaweza pia ukaifanya Yanga itangaze ubingwa mapema zaidi
Mchezo unaofuata kwa Yanga ni Jumatano May 08 dhidi ya Kagera Sugar mchezo huo ukitarajiwa kupigwa katika uwanja wa Azam Complex
Kama Yanga itashinda mchezo huo itafikisha alama 68 ambapo May 13 itakuwa uwanja wa Manungu, Turiani mkoani Morogoro kuikabili Mtibwa Sugar
Ushindi katika mchezo huu utaifanya Yanga ifikishe alama 71 ambazo zinaweza kutosha kuwapa ubingwa kama Azam Fc na Simba zitadondosha alama katika mechi zao zinazofuata
Azam Fc ina alama 57 na inaweza kufikisha alama 72 kama itashinda mechi zake tano zilizosalia wakati Simba inaweza kufikisha alama 71 kutoka katika mechi zake sita zilizosalia
Timu hizo zitachuana May 09 katika uwanja wa Benjamin Mkapa
Azam Fc ndio timu ambayo inaweza kuichelewesha Yanga kutangaza ubingwa lakini kama itapoteza alama katika mechi inazofuata, maana yake Yanga inaweza kutangaza ubingwa May 13 kule Manungu kwani mpaka sasa Yanga ina tofauti ya mabao (GD) 20 zaidi ya yale ya Simba
Ni wazi ushindi katika mechi mbili zinazofuata kwa Yanga unaweza kutosha kutangaza ubingwa au kuhitaji mechi nyingine moja kumaliza kazi