Kocha Mkuu wa Yanga Miguel Gamondi amesema kikosi chake kiko tayari kwa mchezo wa ligi kuu dhidi ya Kagera Sugar ambao utapigwa kesho Jumatano katika uwanja wa Azam Complex
Akizungumzia maandalizi, Gamondi alisema leo timu itafanya mazoezi ya mwisho kuelekea mchezo huo
Gamondi amesisitiza hakuna muda wa maandalizi kutokana na ukaribu wa mechi wanachofanya ni 'recovery' kwa ajili ya kulinda afya za wachezaji
"Tuko tayari kwa mchezo dhidi ya Kagera Sugar hapo kesho natambua mchezo huu utakuwa mgumu kwani Kagera Sugar ni timu nzuri"
"Tunajua tutapata upinzani mkali kutoka kwao, mechi hizi za mwishoni mwa msimu sio nyepesi kwa sababu kila timu inacheza kwa malengo iwe kutwaa ubingwa au kujiokoa na kuteremka daraja"
"Leo tutafanya mazoezi ya mwisho na baada ya mazoezi hayo tutafahamu ni wachezaji gani ambao watakuwa tayari kwa mchezo huo," alisema Gamondi
Aidha Gamondi amesema licha ya kikosi chake kuwa katika nafasi nzuri ya kutwaa ubingwa, kwa sasa hawafikirii ubingwa kwa sababu bado kuna mechi tano za kucheza
"Sisi tunacheza mechi baada ya mechi, hatuwezi kufikiria ubingwa mpaka pale hesabu itakapokamilika. Najua tuna faida ya alama nane juu ya washindani wetu ambao pia watacheza mechi baina yao. Lakini kwa sasa hatuwezi kusherehekea kwa sababu bado kazi hatujaikamilisha"