Kwa sasa hakuna tena uchambuzi kuhusu mbio za ubingwa wa ligi kuu baada ya Yanga kuwa na asimilia 95 za kubeba ubingwa huo
Baadhi ya wachambuzi sasa wamehamia huku kwenye mbio za ufungaji bora, hivi karibuni Bodi ya Ligi ikitangaza kanuni zitakazotumika kumpata mfungaji bora wa msimu huu
Hilo halikufanyika msimu ulopita ambapo Fiston Mayele aligawana tuzo na Saido Ntibazonkiza wa Simba wote wakifunga mabao 17 licha ya Mayele kutokuwa na bao la penati
Wananchi pia wanakumbuka msimu mmoja nyuma jinsi Mayele alivyopigwa zengwe na kunyimwa bao katika mechi ya mwisho na hivyo George Mpole kubeba kiatu baada ya kufunga mabao 17
Wakati huo ilifanyika kampeni kubwa na baadhi ya wachambuzi kumchangia fedha Mpole ili kuhakikisha anaibuka mfungaji bora
Sasa kanuni mpya imeeleza ikitokea kuna wafungaji bora zaidi ya mmoja basi yule aliyefunga mabao machache ya penati atakuwa na faida zaidi kwani bao la penati limepewa alama moja na lisilo la penati limepewa alama mbili
Ikitokea wachezaji hao wakalingana alama baada ya kigezo cha kwanza, kigezo cha pili mwenye faida ni yule aliyecheza dakika chache zaidi
Mpaka sasa Stephane Aziz Ki na Feisal Salum wana idadi sawa ya mabao 15, Aziz Ki ana mabao mawili ya penati wakati Feisal akiwa nalo moja
Kuna watu wanatamani ligi iishe hata leo kwa kuwa mpaka sasa kanuni mpya zinampa faida Feisal kuibuka mfungaji bora kwa kuwa ana bao moja la penati
Hata hivyo bado kuna mechi nne ambazo Aziz Ki anaweza kufanya maajabu yake na kubeba tuzo hiyo
Mara kadhaa Aziz Ki ameweka bayana kuwa jukumu lake ni kuhakikisha anaisaidia Yanga kutwaa ubingwa, suala la tuzo binafsi sio muhimu sana kwake
Lakini ni wazi Wananchi watapenda Aziz Ki abebe tuzo hiyo ili kuweka heshima katika msimu ambao ameonyesha kiwango bora
Akiwa ametwaa tuzo nne za mchezaji bora wa mwezi, Aziz Ki pia ana nafasi kubwa ya kutwaa tuzo ya MVP
