Makamu wa Rais wa Yanga Arafat Haji amewashukuru Wanayanga wote kwa ushirikiano na umoja waliokuwa nao katika kuhakikisha wanatwaa ubingwa wa ligi kuu msimu huu likiwa taji la 30
Arafat amesema wakati wanaingia katika uongozi hakuna aliyedhani kama mafanikio haya yangeweza kupatikana lakini imani na jitihada ni zao la furaha hii ya Wananchi ambao leo wanatembea kifua mbele kutokana na mafanikio ya timu yao
Arafat amesema bado msimu haujamalizika kwani kuna taji jingine linapaswa kurudi mikononi mwao (kombe la Shirikisho la CRDB)
Kupitia ukurasa wake wa mtandao wa kijamii, Arafat ameandika ujumbe huu;
MIZINGA 30 YA SHUKRANI KWA JESHI LA KIJANI, ni kwenye humble beginnings sehemu ambapo ndoto huitwa Jalala, imani huwa rehani, hisia huwa mashakani na furaha ipo taaban, huanza na kuamini kisha kuweka jitihada kufikia malengo.
Ingekuwa masuala ya Kibenki tungesema ‘Mpira Unabenkika’ ndipo ilipoanza hii safari ya Musa na WanaIsrael kuelekea Kaanan, shukrani kwa wote waliotuamini sisi, shukrani kwa Mashabiki na Wanachama, shukrani kwa Benchi la Ufundi, wachezaji na kila mmoja kwenye hii safari ya ubingwa wa 30.
Mizinga 30 ya shukrani inaifanya klabu hii kuwa yenye mafanikio zaidi, ubora zaidi na pasi na shaka Yanga Afrika ni kielelezo cha ubora na uthubutu, bado malengo hayajafikiwa na bado deni ni kubwa sana ila kwa huu mkopo wenu wa iman kwa uongozi basi naamini litaendelea kulipwa kwa mafanikio makubwa.
Focus kubwa kwasasa Wananchi ni michezo iliyosalia kisha michuano ya Federation, bado kuna vituo kadhaa ili kuhitimisha msimu kwa kishindo, haijaisha mpaka iishe, ndizo hizi ndoto za klabu kubwa kama hii tusherehekee kilele cha mafanikio.
ASANTENI SANA kwa vibe, burudani na ladha kuanzia Sokoine, Mbeya mpaka Kirumba, Mwanza,Lake Tanganyika Kigoma na viwanja vyote na sehemu yote mna thamani kubwa sana, asanteni Wananchi kwakuwa nyuma ya hii timu wakati wote.
Tusherehekee wakati huu na kumaliza vyema kilichobaki, kesho haijulikani ila kwasasa wacha niseme mpaka wakati mwingine tena WANANCHI.