Kocha Mkuu wa Yanga Miguel Gamondi amesema mshambuliaji Clement Mzize bado anaendelea kukua hivyo hakuna sababu ya kumuweka katika presha kubwa wakati huu
Mzize ameendelea kuaminiwa na Gamondi ambapo katika mechi mbili za Mpumalanga Cup ambazo Yanga walicheza dhidi ya Augsburg na TS Galaxy, alianza katika kikosi cha kwanza mbele ya washambuliaji wapya Jean Baleke na Prince Dube
Licha ya ukosoaji anaokumbana nao kutoka kwa mashabiki kutokana na ufanisi wake mbele ya lango, Gamondi amesema Mzize anafanya mambo mengi mazuri awapo uwanjani
"Siku zote nasema watu wasimuangalie Mzize kwa kutumia nafasi pekee, huyu ni kijana ambaye tunaendelea kumtengeneza zaidi lakini kuna mambo mengi makubwa anayafanya uwanjani ambayo mashabiki wanaweza wasiyaone"
"Ndio maana mnaona tunaendelea kumtumia kwani kadiri anavyoendelea kucheza ndivyo ataendelea kuimarika na kusahihisha yale ambayo anaonekana hayafanyi kwa usahihi wakati huu," alisema Gamondi
Katika msimu uliopita, Mzize alihusika kwenye mabao 12 ya Yanga kwenye ligi akifunga sita na kutoa pasi sita za mabao
Mzize pia aliibuka kinara wa mabao kombe la Shirikisho la CRDB akifunga mabao matano