Afisa Uhamasishaji wa Yanga Haji Manara amewataka mashabiki wa timu hiyo kuendelea kununua tiketi kuelekea kilele cha wiki ya Mwananchi Jumapili August 04 katika uwanja wa Benjamin Mkapa
Akizungumza katika Mkutano na Waandishi wa Habari aliofanyika Makao Makuu ya Yanga mapema leo, Manara alisema mauzo ya tiketi yanakwenda vizuri na jambo la uhakika ni kuwa wataujaza uwanja wa Benjamin Mkapa
Manara amesema Wananchi wataujaza uwanja wa Mkapa wao wenyewe pasipo janja janja ya ulanguzi wa tiketi
"Niwaambie tu, mauzo ya tiketi yanakwenda vizuri sana, Wananchi endeleeni kununua tiketi tutakwenda kujaza uwanja wa Benjamin Mkapa pasipo kulangua watu"
"Tunafahamu kuna watu wamefanya ulanguzi mkubwa sana jana ili tu wapate sifa ya Sold Out lakini itafahamika siku ya Tamasha lao na letu"
"Kuna watu wamepewa tiketi 5000, wengine 8000 ili wawauzie watu kwa bei kubwa siku ya Tamasha. Sisi hatufanyi mchezo huo, tunataka kila shabiki anunue tiketi kwa kuzingatia utaratibu uliowekwa"
"Tunawapa wanahabari changamoto, pelekeni kamera zenu uwanja wa Benjamin Mkapa Jumamosi na pia mje kwetu muangalie ipi ni sold out ya kweli na ipi ni sold out ya kilanguzi," alisema Manara
Katika hatua nyingine Manara amewatangaza wasanii ambao watatumbuiza katika kilele cha Wiki ya Mwananchi
Harmonize aka Jeshi ndiye atayeongoza burudani kwa Wananchi siku hiyo akishiriana na wasanii wengine kama Mario, Christian Bella, Bilnas, Chois Twins bila ya kumsahau DJ wa Wananchi, Ali B

Harmonize ameandaa wimbo maalum wa hamasa ambao atauachia leo