Kesho Jumapili mchezo wa fainali ya Ngao ya Jamii kati ya Yanga dhidi ya Azam Fc utapigwa uwanja wa Benjamin Mkapa saa 1 usiku
Kocha Mkuu wa Yanga Miguel Gamondi amesema amekiandaa vyema kikosi chake na anaamini ni mchezo ambao vijana wake watakuwa tayari kusaka ushindi ili kutwaa Ngao
Akizungumza katika Mkutano na Wanahabari mapema leo, Gamondi alisema anatambua ugumu wa mchezo huo lakini yeye ni kocha anayependa kucheza aina hizo za mechi
“Napenda kucheza aina hii ya mechi, tumecheza na Simba sasa Azam ni kipimo sahihi kuelekea msimu mpya, tumekuwa na mwendelezo mzuri tokea tumecheza fainali Zanzibar, napocheza na wapinzani wagumu basi unaimarisha zaidi kikosi chako kiushindani, nina matumaini kesho tutacheza vizuri”
“Tumetumia jitihada kubwa kwenye mchezo uliopita, sina wasiwasi na kikosi changu kwani nina kikosi kipana ambacho kinanipa uhuru wa kupanga wachezaji tofauti, nina jua kesho tutakuwa na mchezo mgumu sana lakini nina imani na vijana wangu"
“Huu ni mchezo wa fainali, unapaswa kuwa makini sana, nakumbuka vyema mchezo uliopita pale Zanzibar, tayari tunayo picha sahihi tunapaswa kwenda na mbinu gani dhidi ya Azam Fc, niwahakikishie Yanga Sc ni timu imara sana, ukitazama mchezo uliopita Simba walitengeneza nafasi moja tu kwa sababu tulikuwa imara kwenye kila idara.”
“Tutacheza mchezo wetu kama ambavyo tumekuwa tukicheza mara kwa mara, jambo la muhimu ni kuhakikisha hatufanyi makosa madogo madogo, hatupaswi kuruhusu bao kwenye mchezo huu, jambo zuri ni kuwa timu yangu inacheza zaidi kitimu.”
“Mchezo uliopita Zanzibar Azam Fc walicheza kwa kujihami sana na kwa tahadhari kubwa mno, tulitengeneza nafasi nyingi sana na hatukucheza tofauti na tunavyochezaga, mchezo ujao ni tofauti na ule kwani hivi sasa Yanga Sc tuna vipaji vikubwa sana ambavyo tunaweza kubadilisha matokeo yaliyopita," alisema Gamondi
Akizungumz kwa niaba ya wachezaji wenzake nahodha wa Yanga Dickson Job amesema dhamira ya timu ni kuhakikisha wanapata ushindi dhidi ya Azam Fc hapo kesho
"Dhamira ya wachezaji ni kupambana na kuhakikisha tunapata matokeo sahihi, ukizingatia Azam Fc na sisi umekuwa ni mchezo mgumu sana, tutahakikisha tunapambana kwa asilimia 100 ili kushinda fainali hiyo," alisema