Kocha Mkuu wa Yanga, Miguel Gamondi, amesema moja ya falsafa anazokuja nazo msimu ujao ni kutoruhusu bao kirahisi kwenye mchezo wowote ambao timu yake itacheza
Gamondi ambaye tayari amehifadhi taji la Ngao ya Jamii msimu huu, amesema timu yoyote inayotaka kushinda mchezo wa mpira wa miguu ni lazima kwanza ihakikishe ina safu bora ya ulinzi ili kutoruhusu mabao rahisi na ya kizembe, hivyo msimu huu pamoja na ubora wa kikosi chake, lakini atahakikisha hilo halitokei
Alisema hata kama litatokea, basi iwe ni nadra na sababu inayojitosheleza na si uzembe wa timu au mchezaji mmoja mmoja
"Moja kati ya vitu ambavyo makocha wengi hawapendi ni kuona timu yake inaruhusu mabao kirahisi na kizembe, na tunakwenda kucheza mechi ngumu za kimataifa, Ligi ya Mabingwa Afrika, huko michezo ni migumu na watu wanatumia sana makosa madogo madogo kukuadhibu, hivyo tunaanza kulifanyia kazi kwenye Ligi Kuu," alisema
Hata hivyo, alisema pamoja na hayo yote, lakini hatobadilika kwenye falsafa yake ya kuuchezea mpira na kushambulia, badala yake atawataka wachezaji wake kuwa makini na kushirikiana wanapokuwa wanazuia na wala isitafsiriwe kama atakuwa nyuma ya mpira
"Bado nitacheza vile vile, sitobadilika kiuchezaji, watu wataiona Yanga ile ile ya msimu uliopita na inawezekana ikawa imara zaidi, sisi tunacheza mpira ambao kila mchezaji anashambulia, kila mmoja anakimbia, kila mmoja anajaribu kurudi haraka kukaba tunapopoteza mipira," alisema Gamondi