Kocha wa Yanga, Miguel Gamondi, amesema anataka kuona kazi wanaimaliza kwenye mchezo wao wa kwanza hatua ya awali ya Ligi ya Mabingwa Afrika dhidi ya Vital'O ya Burundi utakaochezwa Jumamosi kwenye uwanja wa Azam Complex, Chamazi, Dar es Salaam
Akizungumza muda mfupi baada ya kumaliza mazoezi yao jana, kocha huyo alisema anataka kuona wanatumia kwa usahihi kila nafasi wanazozitengeneza ili kupata ushindi mnono utakaowapunguzia kazi kuelekea mchezo wao wa marudiano
"Kama nilivyosema awali, hautakuwa mchezo mwepesi, lakini matamanio yangu ni kuona kazi tunaimaliza kwenye mchezo wetu wa kwanza, nataka twende kwenye mchezo wa marudiano tukiwa hatuna presha kubwa," alisema Gamondi
Katika mazoezi yanayoendelea Kigamboni jijini Dar es Salaam kabla ya mchezo wa awali, Gamondi, juzi alikuwa makini mno na mkali kwa washambuliaji wake, Jean Baleke, Prince Dube, Kennedy Musonda na Clement Mzize akiwataka watumie nafasi zinazopatikana kupachika mabao upande wowote ambao mpira utakuwa, mguu wa kulia au wa kushoto
Kitendo cha kocha huyo kuonesha kukomalia safu yake ya ushambuliaji ni kutaka kuona wanatumia nafasi nyingi wanazozitengeneza katika eneo la hatari la wapinzani wao
Tangu kuanza msimu huu, Yanga imeonekana tishio kwenye safu yake ya ushambuliaji, ambapo katika michezo sita waliyocheza tangu wakiwa Afrika Kusini, na miwili ya Ngao ya Jamii ikiwa hapa nchini, imefunga mabao 13, na kuruhusu manne, ambapo katika michezo hiyo sita, wameshinda michezo mitano na kupoteza mchezo mmoja